Serikali imesema itaweka wazi kilichomuua Dk William Mgimwa Jumapili, huku Katibu wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Martini Simangwa akisema marehemu Mgimwa atazikwa Jumatatu katika Kijiji cha Magunga kilichopo Kata ya Maboga mkoani Iringa.
Mwili wa Dk Mgimwa aliyekuwa Waziri wa Fedha,
unatarajiwa kuletwa nchini kesho ukitokea Pretoria, Afrika Kusini.
Mgimwa alifariki dunia katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic iliyoko
Pretoria alikokwenda kwa matibabu.
Wakati hayo yakielezwa, Serikali imeahidi kuweka
wazi kilichomuua Dk Mgimwa wakati wa kumuaga marehemu Jumapili kwenye
Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge,William Lukuvi, alisema
kuwa kwa sasa ni mapema kueleza kilichomuua Dk Mgimwa.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Msemaji wa
familia, Charles Nyato alisema mwili utawasili saa 7.00 mchana kwa ndege
ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na kupelekwa nyumbani kwake
Mikocheni B, Mtaa wa Ruvu.
“Baada ya shughuli ya kuaga, siku hiyohiyo, mwili
utasafirishwa kwa ndege kwenda kijijini, Magunga ukipitia Iringa mjini
kutoa nafasi kwa wananchi kutoa heshima za mwisho kisha kwenda kijijini
ambako mwili utalala kabla ya mazishi Jumatatu,” alisema Nyato.
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amemtumia
salamu za rambirambi Rais Jakaya Kikwete kutokana na kifo cha Waziri wa
Fedha, Dk William Mgimwa.
Katika salamu hizo, Dk Shein amemwelezea marehemu
kwamba atakumbukwa kutokana na utumishi wake uliotukuka kwa Serikali na
wananchi wa Tanzania.
“Tanzania imempoteza kiongozi shupavu, mpenda kazi, mzalendo na mtu mwenye busara na upendo kwa wenzake,” alisema.
Naye mtoto wa marehemu, Godfrey Mgimwa
akizungumzia kifo cha baba yake alisema: “Kifo cha mzee ni pigo kubwa
sana kwetu, inauma ila ndiyo mipango ya Mungu.
“Mzee alikuwa ni mtu anayependa haki na mpenda
maendeleo, kiongozi bora na alikuwa akifanya kazi vizuri serikalini.
Tumempoteza mtu muhimu sana,” alisema Godfrey kwa upole.
“Mzee alikuwa na kawaida ya kwenda kuangalia hali ya afya yake
na alikwenda Afrika Kusini kutokana na mazingira yake ya kazi, lakini
kilichosababisha kifo bado hatukijui,” alisema Godfrey.
Akizungumza na gazeti hili kwenye Ofisi ya Mbunge
iliyopo katika jengo la Siasa ni Kilimo la Halmashauri ya Iringa
Vijijini, Simanagwa alisema mwili utakapowasili utasafirishwa hadi
kijijini kwao Magunga, Kata ya Maboga katika Jimbo la Kalenga ambako
ndiko alikozaliwa. Aidha aliwataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi
hiki kigumu cha msiba
Jirani wa muda mrefu wa Dk Mgimwa, Mbunge wa
Namtumbo Mkoa wa Ruvuma (CCM), Vita Kawawa alisema kifo cha Dk Mgimwa ni
pigo kubwa serikalini, jamii na jimboni kwa jumla.
“Nilimfahamu Dk Mgimwa hata kabla ya kuingia
katika siasa, kipindi najenga vifaa nilikuwa naviacha kwake, inauma sana
kumpoteza mtu muhimu, tutamkumbuka kwa mengi, tumempoteza kipindi
ambapo taifa na wapiga kura wake walimtegemea. Hiyo yote ni mipango ya
Mungu,” alisema Vita
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba alisema:
“Chama na Taifa kimempoteza mtu makini na muhimu kutokana na kuwajibika
ipasavyo, alifufua vyanzo vya mapato vilivyokuwa vimejificha.
“Ameondoka wakati tunamuhitaji...mara ya mwisho
nakumbuka alisema ana matatizo ya figo sasa sijui ndio kilichosababisha
kifo chake au la lakini tusubiri ripoti ya madaktari.”
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
alisema: “Tangu nianze kufanya kazi sijawahi kukutana na kiongozi kama
Dk Mgimwa. Alikuwa kiongozi na msikilizaji wa mawazo yanayotolewa na
wengine, ametufundisha jinsi ya kuwa kiongozi.”
Aliongeza “Tumempoteza mtu muhimu kutokana na
weledi wake katika kazi. Taifa, wapigakura wake na wananchi kwa ujumla
tutamkumbuka kwa uongozi wake madhubuti.”
0 comments:
Post a Comment