Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema mwanachama yeyote anayetangaza nia ya kuwania nafasi ya urais kabla ya muda mwafaka kutangazwa, anapoteza sifa ya kuwa mgombea.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema Dar es Salaam jana kwamba chama hicho kinaamini katika umoja na
mshikamano na kwamba wanaotangaza nia ya kugombea urais kabla ya muda
wamepoteza sifa kwa kuwa ni kama wanakigawa.
Juzi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
alitangaza nia ‘kimtindo’ akisema anaanza rasmi safari aliyoiita ya
matumani ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za Watanzania za
kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Lowassa ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa
wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015,
alitangaza hayo katika ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka mpya, katika
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli.
Nape alisema wanaotangaza nia ya kuwania urais
hivi sasa wanafahamu kwamba hawana sifa za kuwa wagombea wa nafasi hizo
kwa sababu mbalimbali.
Alisema wanafahamu wazi kwamba vikao vya chama havitawapitisha kutokana na kutuhumiwa kwa rekodi zao pia ni mbaya.
“Suala hili liko wazi katika chama chetu, viongozi
wenye sifa waliowahi kuongoza nchi hii hawakujitangaza mapema.
Walisubiri na muda ulipofika wakatangaza nia ya kuwania,” alisema Nape.
Alisema kwa hao wanaojitangaza hivi sasa kabla
muda, wanakigawa chama na kwamba vikao havitawapitisha labda wafanye
hivyo kupitia vyama vingine.
“Labda wagombee urais kupitia vyama vingine lakini
si CCM, chama hiki kina misingi na taratibu zake, wanachama
wanashikamana hadi muda utakapofika,” alisema.
Alisema viongozi bora hawapatikani kwa kujiandaa
wao wenyewe kuchukua nafasi hizo, bali kwa kuombwa na wanachama wenzao
katika hatua mbalimbali zinazokubalika.
Oktoba mwaka jana, Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed
Ali Shein alielezea kushangazwa na tabia ya baadhi ya wanachama wa CCM
kutangaza nia ya kuwania nafasi za uongozi kwa uchaguzi wa 2015 ikiwamo
nafasi ya urais wakati wahusika wa nyadhifa hizo bado hawajamaliza muda
wao.
Akifungua Mkutano wa Makatibu wa CCM wa Mikoa, Dk Shein aliwataka watu hao kusubiri hadi chama kitakapotoa mwongozo.
Katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana kwenye mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini, mwishoni mwa
mwaka jana, alisema wanaotangaza nia mapema, wanajitengenezea mazingira
magumu ndani ya chama.
Mbali na Lowassa, wengine wanaotajwa kuwania
nafasi hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.
0 comments:
Post a Comment