Wakazi na wapita njia katika makutano ya barabara ya Morogoro na Shekilango, jana walikumbwa na hofu kufuatia kuzagaa kwa taarifa ya kuonekana kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu la kutupa kwa mkono ambalo lilikuwa ardhini eneo hilo, jirani na maghorofa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Heka heka hiyo ilizuka kunako saa tano na robo za
asubuhi na kudumu kwa zaidi ya saa moja, kulitokana na mkazi mmoja wa
jijini, Alfani Zidadu kuona kitu kilichokuwa ardhini ambacho
kilishabihiana na bomu hali ambayo ilimfanya awasiliane na mama yake
ambaye alikuwa na miadi ya kukutana nae eneo hilo.
Zidadu alisema kuwa mama yake, Asha Zidadu alikuwa
anakaribia eneo la tukio na alipofika eneo hilo alimuonyesha kitu hicho
na muda mfupi baadae aliwasiliana na polisi Urafiki ambao walifika na
baada ya kukiona kitu hicho walizungushia uzio eneo hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius
Wambura alikiri kuwepo kwa tukio hilo lakini alikataa kuingia kwa undani
kuhusiana na kitu hicho iwapo ni bomu au la kwa madai kuwa polisi
wanakifanyia uchunguzi ili kujua ni kitu gani hasa.
“Kwa sasa siwezi kusema kuwa ni bomu au la
isipokuwa tunasubiri uchunguzi kujua kilikuwa ni kitu gani hasa” alisema
Kamanda Wambura na kubainisha kuwa kwa sasa anaweza kusema kuwa ni
mabaki ya vipande vya mabati.
Mwananchi baada ya kufika katika eneo hilo
lilishuhudia askari wakiimarisha ulinzi katia eno hilo huku wananchi
wakitawanywa na kutakiwa kuwepo mita 100 kutoka eneo la tukio kwa
maelezo kuwa iwapo litalipuka linaweza kusababisha wakapoteza maisha.
“Ondokeni hapa, simameni huko” alisema askari
aliyekuwa ameshika bunduki ya kufyatulia mabomu ya machozi na kuongeza
kuwa wateguaji wangefika eneo hilo wakati wowote na iwapo makosa
yatafanyika wakati wa kulitegua wananchi walio jirani na eneo hilo
wangeweza kupoteza maisha.
Askari wa kikosi maalum cha kutegua mabomu ilifika
eneo hilo na kuanza kazi ya kuchimba na kuweka tahadhari zote za kuzuia
lisilipuke na msimamizi wa operesheni hiyo ambaye al ikataa kutaja
jina lake aliwataka askari wanaotegua kuhakikisha pini ya bomu hilo
imekaza na ipo katika sehemu yake.
“Hakikisheni pini imekaza na hata kama imelegea
irudishieni” alisema msimamizi huyo na baada ya kufukuliwa kwa kitu
hicho kinachodhaniwa kuwa ni bomu, kiliwekwa katika mfuko wa karatasi na
kufungiwa katika sanduku maalum ambalo walifika nalo eneo hilo la
tukio.
Baadhi ya watu waliozungumza na Mwananchi
walionyeha mshangao kuhusiana na kitu hicho na kuhoji kuwa iwapo ni bomu
ambalo limetegwa lilikuwa limemlenga nani kwani wengi wa watu
wanaoshinda eneo hilo ni wale wa bodaboda na abiria wanaosubiria mabasi
ya kwenda Mwenge kupitia Sinza.
“Sijui mlengwa alikuwa nani lakini ni bomu kabisa
kama yale ambayo huwa tunayaona katika luninga” alisema muosha magari
katika eneo hio aliyejitambulisha kwa jina la Ibrahim Momba na kuongeza
kuwa huenda kuna harufu ya ugaidi katrika tukio hilo.
0 comments:
Post a Comment