JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
SEHEMU YA KWANZA
MIPAKA, ALAMA, LUGHA, UTAMADUNI NA TUNU ZA TAIFA
Jamhuri ya
Muungano 1.-(1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho lenye
mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla
ya Hati za Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi
huru.
(2) Jamhuri ya Muungano ni Shirikisho la kidemokrasia
linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu,
kujitegemea, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.
(3) Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyorejewa katika Ibara
ndogo ya (1), ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Katiba hii, kwa kadri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa Makubaliano hayo.
Eneo la Jamhuri ya Muungano
2. Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara
ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha
sehemu yake ya bahari.
Alama na Siku
Kuu za Taifa 3.-(1) Alama za Taifa ni:
(a) Bendera ya Taifa;
(b) Wimbo wa Taifa; na
(c) Nembo ya Taifa,
kama zitakavyoainishwa katika sheria itakayotungwa na Bunge.
(2) Siku Kuu za Kitaifa zitakuwa ni:
(a) Siku ya Uhuru wa Tanganyika, itakayoadhimishwa tarehe 9
Disemba;
(b) Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar, itakayoadhimishwa tarehe 12
Januari;
(c) Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,
itakayoadhimishwa tarehe 26 Aprili; na
(d) Siku Kuu nyingine zitakazoainishwa na sheria za nchi.
(3) Kila Siku Kuu ya Kitaifa itakuwa ni siku ya mapumziko.
Tufuatilie toleo lijalo kujua zaidi
0 comments:
Post a Comment