Maafisa wakuu watendaji wa
kampuni za huduma za simu nchini Kenya wameandikisha taarifa kwa polisi
kuhusu swala la baadhi ya wateja wao kutumia kadi za simu zisizosajiliwa
na ambazo zimehusishwa na uhalifu nchini humo.
Maafisa hao wa kampuni za simu za Safaricom na
Airtel waliandikisha taarifa kuhusu swala hilo baada ya serikali kuonya
kuwa watachukuliwa hatua za kisheria kwa kutohakikisha kuwa wateja wao
wanatumia kadi za simu zilizosajiliwa.Mkuu wa kampuni ya Safaricom, kampuni kubwa zaidi ya huduma za simu nchini humo, Bob Collymore, alihojiwa na maafisa wa ujasusi asubuhi ya leo huku mwenzake wa kampuni ya Airtel Shivan Bhargava akifika kuandikisha taarifa yake asubuhi ya leo pia.
Maafisa hao wamekosolewa kwa kukosa kutii masharti ya kuhakikisha kuwa hakuna mteja hata mmoja anayetumia kadi ya simu isiyosajiliwa.
Hii ni baada ya taarifa kusema kuwa polisi wanajaribu kutafuta nambari za simu zilizotumiwa na watu waliohusika na shambulizi la kigaidi dhidi ya Westgate na kusababisha vifo vya watu 67 huku mamia zaidi wakijeruhiwa.
Mnamo Jumatatu wakuu wa kampuni za huduma za simu na mawakala wao wakionywa kuwa huenda wakakamatwa kwa makosa ya uhalifu na kukosa kusajili kadi za simu za wateja wao.
Waziri wa mawasiliano Fred Matiang'i alisema kuwa polisi wanafanya msako kote nchini kuwatafuta wale wanaokiuka sheria inayoshurutisha usajili wa kadi za simu iwe ni wakuu wa kampuni za simu au mawakala wao.
Kwa mujibu wa tume ya mawasiliano nchini Kenya, zaidi ya watu laki sita wanatumia kadi z simu ambazo hazijasajiliwa kote nchini.
0 comments:
Post a Comment