DSC04577
Rais wa shirikisho la wachimbaji madini Tanzania (FEMATA), John Bina akifungua kikao cha kwanza cha kamati ya dhahabu ya FEMATA Taifa, kilichofanyikia mjini Singida.Wa kwanza kulia na mwenyekiti wa FEMATA Ahmed Adamu na kushoto ni Golden Hainga, katibu wa FEMATA.
DSC04568
Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Singida,Farijala Kiunsi akitoa taarifa yake ya utekelezaji katika kikao cha FEMATA.
DSC04583
Baadhi wa wajumbe wa mkutano wa FEMATA wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa kwenye kikao cha wachimbaji Dhahabu mkoani Singida.
DSC04593
Rais wa FEMATA Taifa, John Bina (wa pili kulia walioketi) akiwa kwenye picha ya pomoja na viongozi wa kitaifa wa FEMATA taifa waliohudhuria kikao mjini Singida.Wa kwanza kulia ni mwenyekiti wa FEMATA, Ahmed Adamu na kushoto ni katibu wa FEMATA,Golden Hainga.(Picha zote na Nathaniel Limu).

RAIS wa Shirikisho la wachimbaji madini Tanzania (FEMATA), John Bina, amewataka wachimbaji madini kujenga utamaduni wa kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha ili fedha wanazozipata ziweze kuwaletea maendeleo endelevu.
 Bina amesema hayo wakati akifungua kikao cha kamati ya dhahabu ya FEMATA taifa, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya madini kanda ya kati mjini hapa.
 Amesema wachimbaji madini wamekuwa na sifa mbaya kwa madai kwamba, wengi hutumia fedha vibaya na kupelekea shughuli ya madini kutokuwanufaisha kimaisha.
 Bina amesema matumizi  hayo mabaya ya fedha, yana madhara mengi ikiwemo mhusika kufilisika mapema.
 “Uzoefu unaonyesha kwamba mchimbaji akipata kwa mfano shilingi milioni 10,kipaumbele chake kinakuwa ni  kuoga mwili kwa  pombe (bia), ataacha kuchimba madini na kutumbukia kwenye anasa hadi hapo fedha zitakapomwishia”,alifafanua Rais huyo.
 Kwa hali hiyo,Bina aliwataka wabadilike na kuwa na nidhamu nzuri ya matumizi ya fedha, ili fedha wanazozipata ziwasaidie kujiletea maendeleo wao binafsi,familia zao,mkoa wao na taifa kwa ujumla.
 Katika hatua nyingine, Rais Bina aliwataka wachimbaji madini kujiepusha na uchimbaji haramu na pia wajenge utamaduni wa kulipa kodi, ili kujijengea mazingira ya kukopesheka na taasisi za kifedha.
 Wakti huo huo, kikao hicho kilimteua Farijala Kiunsi kuwa katibu wa FEMATA Taifa.