Friday, December 6, 2013

DR. SLAA APOKEWA KWA MABANGO YENYE UJUMBE MZITO KIGOMA

http://azizicompdoc.blogspot.com/
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbrod Slaa amepokewa kwa mabango katika mkutano wake wa hadhara wilayani Kakonko, Kigoma lakini akawaambia waliofanya hivyo kuwa chama chake hakitayumbishwa huku akiwataka wanaosimama na mabango kumtetea Zitto Kabwe kung’oka naye ndani ya chama.
Dk Slaa yuko mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 11 kutembelea Mikoa ya Shinyanga na Kigoma kukagua na kuimarisha uhai wa chama.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mwenge Kakonko, Dk Slaa alisema Chadema ni chama imara na kinaendeshwa kwa misingi ya katiba na kanuni.
“Hakuna kiongozi aliye juu ya katiba, ninawaasa wote wanaobeba mabango kujiangalia kwa kuwa ninafahamu wanatumiwa.”
Kabla ya kupokewa kwa mabango hayo, Dk Slaa aliyewasili Kakonko saa 5:11 asubuhi akitokea Wilaya ya Kahama, Shinyanga alikwenda moja kwa moja katika Kata ya Mhange ambako alifanya mkutano wa hadhara.
Dk Slaa alikumbana na mabango hayo saa 8:45 mchana msafara wake ulipowasili Kakonko Mjini ukitokea Mhange.
Wakati Dk Slaa akiingia katika uwanja wa mkutano, ulio jirani na Ofisi za CCM Wilaya ya Kakonko, kuliibuka kundi la vijana wapatao watano wakiwa na mabango mkononi na kuanza kukimbia kuyafuata magari matatu ya msafara wa Dk Slaa huku wakionyesha mabango yao. Hatua hiyo iliwafanya polisi waliokuwapo eneo hilo la mkutano kuwazuia na kuanza kuwatimua lakini mara baada ya Dk Slaa kuteremka katika gari yake na kuingia uwanjani hapo, aliomba kipaza sauti na kuwataka askari hao kuacha kuwatimua wenye mabango. “Naomba msiwaondoe waacheni waje... waruhusuni kwenye mkutano na mabango yao. Waacheni waje hapa … msiwazuie, waacheni waonyeshe mabango yao na muwaruhusu tu wapite hapa mbele, msiwapige tafadhali,” alisema Dk Slaa.
Baada ya kauli hiyo, polisi waliwaruhusu vijana hao watano ambao walibakiwa na mabango manne, moja likiwa limechanika walipokuwa wanawazuia.
Mabango hayo yaliyokuwa na maandishi ya aina moja, yalikuwa na ujumbe uliosomeka: “Tanzania Kigoma Kakonko bila Zitto Haiwezekani”, ‘Mhe. Slaa, Mhe. Mbowe mnatakiwa kujiuzuru mara moja” na jingine lilisomeka; “Hatupo tayari kwa kusikiliza lolote bila ya Zitto”.
Mara baada ya kupanda jukwaani Dk Slaa aliwataka tena wenye mabango kusogea karibu na jukwaa kuu alipokuwa amesimama na kuanza kuwauliza maswali vijana hao iwapo wanajua Katiba ya Chadema na kama wana kadi za chama. “Naomba niwaulize, hivi nyie wenye mabango mnaijua Katiba ya Chadema?” Walimjibu: “Hapana.” Dk Slaa akawauliza tena: “Sasa mnadai nini kwa mabango yenu kama hamjui Katiba ya Chadema?”
Mmoja wa walioshika mabango hayo alijibu: “Mtetezi wetu Zitto.”
Kutokana na hali hiyo Dk Slaa aliwauliza, atakuwa amekosea akiwakabidhi kwa Polisi kuwa siyo wanachama wa Chadema lakini wanafanya vurugu katika mkutano halali?
Kabla ya kutoa majibu, baadhi ya wanachama na mashabiki wa Chadema walimbaini kuwa mmoja wa waliobeba mabango hayo anafahamika na ni mtoto wa mmoja wa viongozi wa CCM, hatua ambayo iliwafanya watu waliokuwa wakisikiliza kuanza kumzomea na vijana hao kuinuka na kuanza kuondoka huku wakiendelea kuzomewa.
Baada vijana hao kuondoka, Dk Slaa aliendelea na mkutano huku akiwaeleza wanachama wake kuwa kama wanafikiri kufanya hivyo kunamsaidia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe wanakosea.
Dk Slaa alimnanga Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuhusiana na kilio chake cha mawaziri mizigo akisema hakupaswa kulalamikia majukwaani, bali alitakiwa kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuwatimua mara moja.
“Kinana kulalamika jukwaani haisaidii, hii inaonyesha udhaifu wa CCM ambayo Serikali ndiyo inayotekeleza ilani yake,” alisema Dk Slaa. Dk Slaa alisema pia kuwa Chadema kitatumia wabunge wake kuibana Serikali kuhusu fedha za ruzuku ya kilimo zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo lakini zimekuwa zikitafunwa na wajanja wachache.

Mpasuko wa kisiasa ndani ya Chadema katika Tawi la Mwandiga, Jimbo la Kigoma Kaskazini mkoani Kigoma ulioibuka baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kumvua madaraka Zitto ambaye pia ni mbunge wa jimbo hilo, haujapata suluhu.
Wakati hali ikiwa hivyo, kuna taarifa za chini kwa chini kuwa baadhi ya viongozi wamekwepa kuungana na Dk Slaa katika ziara hiyo.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa, Jafari Kasisiko hayumo kwenye msafara huo kwa kuwa ni mgonjwa wakati Katibu wa Mkoa, Msafiri Wamalwa yupo mkoani Tabora kwa shughuli za kifamilia.
Mwenyekiti wa Jimbo la Kigoma Kaskazini (Chadema), Ally Kisala alisema uongozi wa jimbo hilo unaendelea na mikakati ya kumpokea Dk Slaa anayetarajiwa kufanya mikutano jimboni humo Desemba 10, mwaka huu.
Kisala alisema uongozi wa Chadema ulipendekeza mkutano huo ufanyike katika Kijiji cha Nyarubanda lakini chama ngazi ya taifa kimeagiza ufanyike Mwandiga, kijiji ambacho kinaonyesha upinzani dhidi ya ziara hiyo.
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limesema limeandaa ulinzi wa kutosha kuhakikisha usalama katika kipindi chote cha ziara ya Katibu Mkuu huyo wa Chadema.

Kikao kilichofanyika chini ya Mwenyekiti wa Chadema Tawi la Mwandiga, Kudra Maulid kwa lengo la kuondoa tofauti zilizojitokeza miongoni mwa wanachama, kilishindwa kupata suluhu baada ya kila upande kuushutumu mwingine kuhusika na mpasuko ndani ya chama.
Mvutano ndani ya tawi hilo uliibuka Novemba 24, mwaka huu, siku mbili tu baada ya Kamati Kuu kumvua Zitto nyadhifa zake pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Hatua hiyo iliwakera baadhi ya wanachama na wapenzi wa Chadema katika tawi hilo ambao waliandamana na kufanya ghasia.
Katika kikao cha juzi, wanachama walijadili hatima ya mgogoro huo na madhara yanayoweza kutokea kwa maslahi ya chama na hivyo kufikia uamuzi wa kuzika tofauti zao licha ya kila upande kushikilia kwamba upo sahihi.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa wanachama hao walikubaliana kuimarisha chama bila kujali kwamba Zitto ni mzaliwa wa kijiji hicho.
Quantity : Add to Cart

2 comments:

  1. Chama kinachokufa ni ccm.Hebu tazama kwa umakini utaona ccm inatumia nguvu kubwa kupambana na chadema na utaona nguvu yao ccm imegonga mwamba wakina chadema wameshituka mapema na kuwafyeka wasaliti ambao wangekiangamiza chama. ukitazama pia kwa umakini hiliswala utaona limewaogopesha sana ccm. chadema itavuka hiki kikwazo na itachukua dola 2015 kirahisi ccm hawajui wanaipigia debe chadema ishinde kwa vitendo vyao vinavyo onekana waziwazi kama vile kuandaa watu kwa garama kuharibu mikutano ya chadema huko kigoma,kuwanunua wakina zito,kitila, said arfi na wengine wengi nasema wengi kwa sababu pesa aliyopewa zito aliitumia kuwannua viongozi wandamizi wa chadema mikoani. mfano juzi hivi nikiwa ndani sa usafiri mjadala ukaanza 99% wakaunga mkono maamuzi ya kamati kuu chadema mmoja alikuwa akipinga sana basi lote lilimshambulia sana akapigwa swali kwa jinsi alivyokuwa amepaniki akalopoka msaada aliopatiwa na zito mil12 + ushauri wa kibiashara na akajitambulisha yeye ni diwani wa kahama(nyasubi). Hapa ccm wanajichanganya tu watanzania 99% tunaona na tutawapiga chini vibaya kwa aibu!!!

    ReplyDelete
  2. Chama kinachokufa ni ccm.Hebu tazama kwa umakini utaona ccm inatumia nguvu kubwa kupambana na chadema na utaona nguvu yao ccm imegonga mwamba wakina chadema wameshituka mapema na kuwafyeka wasaliti ambao wangekiangamiza chama. ukitazama pia kwa umakini hiliswala utaona limewaogopesha sana ccm. chadema itavuka hiki kikwazo na itachukua dola 2015 kirahisi ccm hawajui wanaipigia debe chadema ishinde kwa vitendo vyao vinavyo onekana waziwazi kama vile kuandaa watu kwa garama kuharibu mikutano ya chadema huko kigoma,kuwanunua wakina zito,kitila, said arfi na wengine wengi nasema wengi kwa sababu pesa aliyopewa zito aliitumia kuwannua viongozi wandamizi wa chadema mikoani. mfano juzi hivi nikiwa ndani sa usafiri mjadala ukaanza 99% wakaunga mkono maamuzi ya kamati kuu chadema mmoja alikuwa akipinga sana basi lote lilimshambulia sana akapigwa swali kwa jinsi alivyokuwa amepaniki akalopoka msaada aliopatiwa na zito mil12 + ushauri wa kibiashara na akajitambulisha yeye ni diwani wa kahama(nyasubi). Hapa ccm wanajichanganya tu watanzania 99% tunaona na tutawapiga chini vibaya kwa aibu!!!

    ReplyDelete

Labels

Blogroll

Labels

About