Waraka unaodaiwa kuandaliwa na CCM kwa ajili kuwaelekeza wajumbe wake kwenye Bunge Maalumu la Katiba kutetea msimamo wa Serikali mbili umepokewa kwa hisia tofauti huku Rais Jakaya Kikwete akitakiwa kujitokeza hadharani kueleza msimamo wake.
Waraka huo uliibuliwa na Blog hii jana
ukibainisha sura ya Serikali mbili inayotakiwa na CCM, likiwamo
pendekezo la kuanzisha Baraza la Wawakilishi la Tanzania Bara.
Miongoni mwa waliozungumzia waraka huo ni Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa ambaye amemtaka Rais Kikwete ambaye
pia ni Mwenyekiti wa CCM kutoka hadharani na kuweka wazi msimamo wake
kuhusiana na mchakato wa Katiba Mpya.
Dk Slaa alieleza kushangazwa kwake na hatua ya CCM
kuandika waraka aliodai umebadili vipengele vyote muhimu katika Rasimu
ya Pili ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya
kukusanya maoni kwa wananchi.
Pia amemtaka Rais Kikwete kutozindua Bunge Maalumu
la Katiba linaloendelea mjini Dodoma kwa madai kwamba kiutaratibu,
linajitegemea na hata katika historia ya Katiba zilizowahi kuandikwa
hazijawahi kusainiwa na rais.
Dk Slaa alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea ubunge katika Jimbo la
Kalenga, Iringa kupitia Chadema, Grace Tendega uliofanyika katika Kijiji
cha Tanangozi, Kata ya Mseke.
Alisema Rais Kikwete na chama chake wanataka
kubadili mambo yote muhimu yaliyoandikwa katika Rasimu ya Pili
inayojadiliwa mjini Dodoma, huku akijua kuwa zaidi ya asilimia 60 ya
Watanzania ndiyo waliotoa maoni.
Wengine wauponda
Mjumbe wa Bunge la Katiba, James Mbatia alisema
ushawishi katika jambo lolote siyo dhambi, lakini hakutarajia ushawishi
huo kufanywa na CCM, tena katika jambo nyeti kama mchakato wa Katiba.
“Kama suala ni Serikali tatu, hayakuwa mapendekezo
ya Jaji Warioba, bali ya tume nyingi zilizowahi kuundwa na Serikali
inayotokana na chama hicho tawala. Kuna Tume za Jaji Robert Kisanga,
Francis Nyalali, William Shelukindo, Amina Salum Ali na sasa Joseph
Warioba. Zote hizi zimependekeza Serikali tatu.”
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema
CCM kutengeneza waraka huo ni sawa na `utekaji nyara’ wa maoni ya
wananchi na kuweka maoni ya wana CCM katika Katiba Mpya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema kitendo cha CCM
kutengeneza waraka wake ni kukwamisha upatikanaji wa Katiba bora.
“Hakukuwa na sababu ya kuweka Tume ya Mabadiliko ya Katiba iwapo
nao wanakuja na waraka wao, tunatakiwa kuboresha yaliyomo kwenye rasimu
ili tuweze kupata Katiba yenye maoni ya watu,” alisema.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Gaudence Mpangala alisema iwapo CCM kimesambaza waraka huo, kinafanya
makosa kwa kuendeleza misimamo isiyokuwa na hoja za msingi kwa
Watanzania... “CCM kusambaza waraka huo ni dalili mbaya za kuleta
machafuko miongoni mwa wajumbe...”
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
Tanzania (Tucta), Nicholas Mgaya alisema hatua ya CCM kusambaza waraka
huo ni kutapatapa kwa kuwa yaliyomo hayatawezekana kupitishwa na
Watanzania.
Mgaya alisema waraka huo umevunja Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayozuia kusambaza maoni ya makundi katika mchakato huo.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba
alisema tatizo siyo kuwa na msimamo wa chama kupitia waraka huo, bali
kuusambaza... “Sijaupata waraka huo lakini kitendo cha kuusambaza tu
kisheria ni makosa, walitakiwa kutumia nafasi na wajumbe wake kupeleka
hoja hizo bungeni,” alisema Kibamba.
Wabunge CCM wanena
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema katika
hali ya kawaida, kila kundi katika jamii lina fikra zake kuhusu
mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na haki ya kupendekeza kile
ambacho linaona kinafaa kuongezwa au kuondolewa na kwamba kuwa na
mtazamo tofauti kuhusu jambo fulani ni kitu ambacho hakizuiliki.
“Binafsi ningependa kupata waraka kutoka kila
kundi ili nisome na kujua mawazo mazuri yaliyopendekezwa. Ukipitia ni
wazi kuwa utakutana na mambo mazuri tu. Hili ni jambo ambalo lipo wazi
kabisa.”
Hata hivyo, Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM) alisema chama hicho hakijagawa rasimu yoyote.
Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangalla alisema hana hakika iwapo waraka huo umesambazwa kwa wajumbe.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy naye alisema
hajauona waraka huo, kauli ambayo iliungwa mkono na Mbunge wa Muleba
Kaskazini, Charles Mwijage.
Jana, Blog hii ilichapisha taarifa za
kuonekana kwa waraka huo, ambao pamoja na mambo mengine, umetoa
mapendekezo katika ibara 42 za Rasimu ya Katiba ya Tume na kupangua hoja
mbalimbali ikiwamo ya muundo wa muungano huku ikitaka mfumo wa Serikali
mbili uendelee lakini ufanyiwe marekebisho.
0 comments:
Post a Comment