Ghorofa nne za kisasa zilizopo Dar es Salaam, zinatumia kiasi kikubwa cha umeme kuliko ule unaotumiwa katika Mkoa wa Mtwara.
Majengo manne ya PSPF Twin Tower, Uhuru Height,
Viva Tower na Benjamin Mkapa Tower yote kwa pamoja yanatumia megawati 12
za umeme wakati mkoa huo unatumia megawati nane.
Kiasi hicho cha umeme kinachotumiwa na majengo hayo ni karibu sawa na umeme unaotumiwa na mkoa huo na Lindi kwa pamoja.
Aidha, majengo matatu ya PSPF Twin Tower, Uhuru
Height na Viva Tower kwa pamoja yanatumia umeme mwingi kuliko ule
unaotumiwa na baadhi ya mikoa nchini kama Ruvuma, Manyara, Singida,
Kigoma na Rukwa.
Akizungumza katika mahojiano maalumu hivi
karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania Tanesco,
Felchesmi Mramba alisema PSPF peke yake linahitaji megawati tano na
Uhuru Height megawati 2.5, Viva Tower megawati 2.5 na Benjamin Mkapa
Tower megawati mbili.
Alitaja matumizi ya umeme katika mikoa hiyo na
megawati zake kwenye mabano kuwa ni Manyara (10) Mtwara (8), Singida
(7), Lindi (5.5), Kigoma (6), Ruvuma (4.7) na Rukwa (6.8).
Alisema Dar es Salaam inaongoza kwa kutumia umeme
mwingi na kwamba mahitaji ya nishati hiyo yamekuwa yakiongezeka kutokana
na ukuaji wa haraka wa sekta ya ujenzi.
Dar es Salaam pekee, kwa mujibu wa takwimu za
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) matumizi yake ni kati ya megawati
450 na 500 kwa siku, kiasi ambacho ni zaidi ya nusu ya umeme
unaozalishwa na shirika hilo.
Alisema hivi sasa umeme unaozalishwa ni wastani wa
megawati 1,100, huku sehemu kubwa ya nishati hiyo ikitokana na mitambo
inayotumia gesi na mafuta.
Kutokana na hali hiyo, alisema Tanesco imeamua
kutekeleza miradi 13 ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme
ikiwamo kuongeza uwezo wa njia za kusambaza na kukarabati. Pia kujenga
vituo vipya vya kupozea umeme katika sehemu mbalimbali za Dar es Salaam.
“Baadhi ya majengo makubwa Dar es Salaam
yanahitaji umeme mwingi. Unakuta jengo moja kama haya maghorofa
linahitaji megawati nyingi za umeme kuliko zinazotumiwa na baadhi ya
mikoa,” alisema Mramba na kuongeza:
“Ndiyo maana tunatekeleza miradi mingi ya kuongeza
uwezo wa njia za kusambaza umeme maana mfumo tulionao sasa ni chakavu
na hauwezi kuhimili kiasi cha umeme kinachotakiwa na watumiaji wa
makundi mbalimbali.”
Mramba alisema uchakavu wa miundombinu na mahitaji makubwa ya
umeme ni miongoni mwa sababu za umeme kukatika ovyo na kwamba njia za
kuusafirisha hazina uwezo wa kuhimili kiasi kinachotakiwa.
Ili kukabiliana na hali hiyo, alisema shirika lake
linatekeleza miradi inayojumuisha ukarabati wa vituo vya kusambaza
umeme ambao utahusisha vituo vikubwa na vidogo katika maeneo ya
Mwananyamala, Jangwani Beach, Kigogo, Tegeta, Muhimbili, Luguruni,
Mikocheni, Kurasini, Mbagala, Gongo la Mboto na Kipawa.
Mramba alisema Kituo cha Gongo la Mboto
kitahudumia wakazi wa Wilaya ya Kisarawe, Pwani, Segerea na Kinyerezi na
katika Kituo cha Kipawa, Tanesco itaweka ‘saketi’ mbili kutoka Ubungo
ili kutosheleza mahitaji ya viwandani na kusaidia kuwapo kwa umeme
wakati wote endapo njia (line) moja itapata hitilafu.
“Njia (line) nyingine itaanzia kwenye Kituo cha
Ilala, karibu na TBL kwenda katikati ya jiji mpaka Makumbusho na kurudi
Ubungo. Mradi huu utakamilika Aprili, mwaka huu.
Pia utahusisha eneo la Mwenge, Tandale, Mikocheni, Masaki, Oysterbay ili wakazi wa maeneo hayo wapate umeme wa uhakika,” alisema.
Pia utahusisha eneo la Mwenge, Tandale, Mikocheni, Masaki, Oysterbay ili wakazi wa maeneo hayo wapate umeme wa uhakika,” alisema.
Pamoja na vituo hivyo, Tanesco inajenga kituo cha
kisasa eneo la Mikocheni, ambacho kitatumika kubaini maeneo yenye
matatizo katika njia za usambazaji wa umeme... “Hivi sasa line (waya) ya
umeme ikikatika, hatuwezi kujua tatizo liko wapi mpaka mafundi wetu
wafuatilie na kufika katika eneo husika, lakini kituo hiki kitatuwezesha
kutumia mfumo wa kompyuta kuonyesha eneo lenye kasoro.”
Habari zaidi soma Jarida la Uchumi ndani.
0 comments:
Post a Comment