Polisi Kikosi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wamemkamata mkazi wa Temeke, Mwanahamisi Salim (27) kwa tuhuma za kumeza kete 71 za dawa za kulevya aina ya heroini zenye thamani ya zaidi ya Sh60 milioni.
Mkuu wa Upelelezi wa Viwanja vya Ndege Tanzania,
Hamad Hamad alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa alasiri ya Februari 20,
mwaka huu akijiandaa kupanda Ndege ya Shirika la Emirates kwenda Hong
Kong, China.
“Tulipomhoji alitueleza kuwa dawa hizo alikuwa
anazipeleka kwa marafiki zake kutoka Nigeria ambao wanaishi Hong Kong
lakini bado tunaendelea kumhoji ametoa wapi huo mzigo,” alisema Hamad.
Alisema katika siku za karibuni, wamebaini kuwa watuhumiwa wengi wanaokamatwa ni wanawake.
Alisema wengi wa wanawake hao wanadai wanakwenda kununua vifaa vya saluni.
Kamanda wa Polisi, Kitengo cha Kupambana na Dawa
za Kulevya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Godfrey Nzowa
alisema dawa zilizokamatwa ni heroini.
Katika hatua nyingine; taswira ya Tanzania
imeendelea kuchafuka baada ya Kituo cha Kimataifa cha Televisheni cha
France 24 kutoa ripoti inayoonyesha ukubwa wa tatizo la dawa za kulevya
nchini.
Ripoti hiyo inakuja zikiwa zimepita wiki mbili
tangu Gazeti la The Mail on Sunday kuandika habari za kukithiri kwa
ujangili wa meno ya tembo na pembe za faru.
Taarifa ya kituo hicho ilieleza kuwa Tanzania inaonekana kuwa kituo cha dawa za kulevya kutoka Afghanistan na Pakistan.
Mmoja wa waandishi walioandaa ripoti hiyo, Jaouhar
Nadi alisema tatizo la dawa za kulevya Tanzania ni kubwa na hakuna
mikakati ya makusudi ya kupambana nalo.
“Zanzibar kwa mfano, kuna watumiaji 10,000 wa dawa
za kulevya, yaani katika kila familia moja kuna mteja mmoja. Kuna
‘mateja’ wapatao 250,000 nchi nzima na jitihada za Serikali zinaonekana
kuwa dhaifu,” alisema Nadi alipokuwa akihojiwa na France 24 na kuongeza:
“Zanzibar kwa mfano, hakuna programu yoyote ya Serikali zaidi ya ile
iliyoanzishwa na taasisi ya Kimarekani.”
Nadi alisema licha ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuanzisha
Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, bado uingizwaji wa dawa hizo
umekithiri.
“Mamlaka zinashughulikia suala hilo, walianzisha
tume miaka ya 1990. Hata hivyo, usafirishaji wa dawa za kulevya bado ni
mkubwa,” alisema na kuongeza:
“Inakadiriwa kuwa biashara hiyo huingiza zaidi ya
Dola 165 milioni na tani 22 za heroini huingizwa nchini humo kila mwaka.
Hizo ni fedha nyingi na watu wanaamini kuna rushwa hasa kwa viongozi wa
juu na wabunge.
“Majina ya wakubwa wanaohusika na biashara hiyo yanafichwa. Wengi wanaamini ni kazi ya wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo.”
Akizungumzia madai hayo Kamanda Nzowa alipinga
utafiti huo na kusema jitihada kubwa zimefanyika... “Kama ni kweli kuna
tatizo kubwa kiasi hicho, hao waandishi walipaswa watuambie dawa hizo
zinauzwa bei gani, kwa sababu ninavyojua ni kwamba, huko mitaani dawa
zinauzwa bei ghali mno. Kilo moja inafikia hadi Sh50 milioni, sasa
utasemaje kwamba matumizi ya dawa yameongezeka?”
“Ni kweli tatizo la dawa za kulevya lipo, pia
ukamataji ni mkubwa. Kwa mfano, mwaka jana tu tumekamata kilo 1,882 za
heroini. Februari 4, mwaka huu tumekamata kilo 201 na wenzetu
wanaodhibiti baharini wamekamata kilo 350 za dawa hizo. Hiyo pekee
inajenga hofu kwa waingizaji. Itakuwaje waendelee kuleta?”
Alisema majina ya watu wanaohisiwa yamekuwa
yakifanyiwa kazi ikiwa pamoja na kuwafikisha mahakamani... “Mwaka jana
kuna gazeti moja la Kiswahili lilifanya utafiti na mimi pia nilizungumza
nao. Baada ya hapo tulikamata watu 266. Baada ya kuwapekua hatukuwakuta
na ushahidi, lakini bado tuliwafikisha mahakamani kwa kuwa walikuwa na
dalili za kuhusika,” alisema na kuongeza:
“Tunapata taarifa mbalimbali na tunawashukuru
wananchi, lakini wanapaswa watupe kwa siri siyo kutangaza hadi wahusika
washtuke. Hii ni vita ya dunia nzima, siyo Tanzania tu.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Zanzibar, Mohamed Aboud alisema hana taarifa za kutosha kuhusu utafiti
huo, lakini hali siyo mbaya kiasi hicho.
“Ni kweli kuna tatizo la dawa za kulevya hapa
Zanzibar na watu wengi wameathirika, lakini sidhani kama ni kwa kiasi
kikubwa hivyo. Bado tunafuatilia utafiti huo ili kujiridhisha na kutoa
taarifa rasmi,” alisema Aboud.
0 comments:
Post a Comment