Siku moja baada ya Rais Yoweri Museveni kusaini sheria inayotoa adhabu kali kwa wapenzi wa jinsi moja, Marekani imesema inaangalia upya uhusiano wake na nchi hiyo kama ilivyoainisha awali.
Katika taarifa yake iliyotolewa jijini Washington
DC jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry alisema Serikali
ya Rais Barack Obama itahakikisha ushirikiano wowote na Uganda
utachujwa kupitia sheria za kupinga ubaguzi ambazo inazisimamia.
“Sheria imeshapitishwa, tunaanza kuchuja uhusiano
wetu na Uganda kwa kuangalia mambo muhimu, ikiwemo maeneo
tunayowawezesha,” alisema Kerry katika taarifa yake jana.
Awali, akitia saini muswada huo kuwa sheria juzi,
Rais Museveni alipuuza vitisho vya Marekani na kusema mataifa ya nje
ambayo yamekuwa yakimtaka asisaini muswada huo pamoja na viongozi wa
kidini hawana nafasi katika mambo ya ndani ya nchi yake.
“Watu kutoka nje hawawezi kutuamuru tufanye au
tusifanye mambo yetu. Kama hawataki kwenda nasi, basi wanaweza kuchukua
misaada yao,” alisema.
Akizungumzia onyo lililotolewa na baadhi ya
viongozi wa kidini akiwemo Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini,
Museveni alisema: “Kumbuka hata Yesu aliuawa na maaskofu, ndiyo maana
huwa sisikilizi watu hao (viongozi wa kidini).”
Wakati Marekani na baadhi ya washirika wao
wakitishia kuzuia misaada kwa Uganda, mataifa mengi ya Afrika, isipokuwa
Afrika Kusini yana sheria kali za kupiga marufuku wapenzi wa jinsi
moja. Sheria zimekuwa zikitekelezwa kwa muda mrefu sasa.
Shirika la Haki za Binadamu, Amnesty International
linasema uhusiano wa kimapenzi wa watu wa jinsi moja umeharamishwa
kisheria katika nchi 38 kati ya 54 barani humo na adhabu ya kifo
imehalalishwa nchini Mauritania, Sudan na Somalia.
Nchi zilizoweka sheria kali kuwabana wapenzi wa
jinsi moja ni pamoja na Uganda ambayo imepiga marufuku wapenzi wa jinsi
moja na kutoa adhabu ya hadi kifungo cha maisha gerezani kwa wale
wanaorudia vitendo hivyo.
Sheria hiyo inazuia kutangaza masuala yahusuyo wapenzi wa jinsi moja na kuwataka watu kuwatenga na kuwakataa mashoga.
Nigeria, pia imeweka sheria maalumu iliyoanza
kutekelezwa Januari mwaka huu. Sheria hiyo inatoa adhabu ya kifungo cha
hadi miaka 14 jela kwa wapenzi wa jinsi moja wanaoishi pamoja
Pia, inatoa kifungo cha hadi miaka 10 kwa kuonekana hadharani wakijiachia kama wapenzi.
Katika eneo la Kaskazini linalotawaliwa chini ya sheria za Kiislamu, wapenzi hao wanakabiliwa na adhabu ya kifo.
Cameroon ni miongoni mwa nchi zenye sheria za aina
hiyo, ambapo wapenzi wa jinsi moja wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi
miaka mitano jela.
Gambia imekuwa na mfumo wa sheria dhidi ya wapenzi wa jinsi moja wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 14 jela na kazi ngumu.
Nchini Zambia pia, wapenzi wa jinsi moja walipigwa
marufuku tangu enzi za utawala wa Waingereza na waliobainika,
walikabiliwa na kifungo cha hadi miaka 14 jela.
Kwa upande wa Senegal, yeyote atakayetiwa hatiani
kwa kujihusisha na kitendo chochote kisichokuwa cha asili na mtu wa
jinsi yake anakabiliwa na kifungo cha miaka mitano jela.
Nchini Tunisia, vitendo vya uhusiano ya wapenzi wa jinsi moja kwa watu wazima hukabiliwa na adhabu ya hadi miaka mitatu jela.
Nako Morocco, wenye tabia hiyo hukabiliwa na kifungo cha kuanzia miezi sita hadi miaka mitatu jela.
Kule Algeria, yeyote anayetiwa hatiani kwa
kujihusisha na mapenzi ya jinsi moja anakabiliwa na adhabu ya kifungo
cha miaka miwili jela, lakini wengi huweza kushikiliwa kwa muda
usiojulikana.
Nchini Zimbabwe, Rais Robert Mugabe amekuwa akisisitiza kwamba wapenzi wa jinsi moja ni wabaya kuliko nguruwe na mbwa.
Hata hivyo, inadaiwa kwamba makundi ya watu wa aina hiyo yanaruhusiwa katika baadhi ya maeneo.
Nako Malawi, Novemba mwaka 2012, Rais Joyce Banda
alizuia sheria za kupiga marufuku wapenzi wa jinsi moja hadi
zitakapojadiliwa bungeni. Kwa sheria iliyopo, wanaume wanakabiliwa na
kifungo cha hadi miaka 14 jela na wanawake hadi miaka mitano jela.
Nchi nyingine zikiwamo Chad, Gabon, Ivory Coast na Mali
hazijapiga marufuku, lakini Afrika Kusini iliruhusu ndoa za jinsi moja
mwaka 2006.
Pamoja na hatua hiyo, wapenzi wa jinsi moja
wamekuwa wakidhibitiwa ipasavyo kwa kuadhibiwa iwe wanaume au wanawake
ili kuwarejesha kwenye mfumo wa kawaida.
Jarida moja nchini Uganda limechapisha orodha ya
majina na watu 200 liliowataja kuwa wapenzi wa jinsia moja, siku moja
baada ya Rais Yoweri Museveni kutia saini sheria inayowabana watu wa
namna hiyo.
Jarida hilo lililopewa jina la Red Pepper
lilichapisha majina hayo jana pamoja na picha za wahusika katika ukurasa
wake wa mbele, chini ya kichwa cha habari: “WAANIKWA!”
Orodha hiyo inajumuisha wanaharakati maarufu wa
haki za mashoga wa Uganda, akiwemo Pepe Julian Onziema ambaye mara
kadhaa alionya kwamba sheria hiyo ya kuwabana wapenzi wa jinsi moja
itaibua machafuko. Msemaji wa Polisi wa Uganda, Patrick Onyango alisema
hata hivyo hakuna wahusika waliokamatwa tangu Rais Museveni alipotia
saini sheria hiyo juzi, lakini tayari hakuna msalie mtume kwa wale
watakaotiwa nguvuni.
Akitia saini muswada huo kwenye Ikulu ya Eenrebbe
mbele ya wanahabari na maofisa wa juu wa Serikali yake juzi, Museveni
mbele ya maofiosa wa juu wa Serikali yake na waandishi wa habari,
alisema adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa wale watakaopatikana na
hatia kwa mara ya kwanza haiepukiki. Pia, adhabu ya maisha jela
itatolewa kwa watu watakaopatikana na hatia ya kushiriki mapenzi ya
jinsia moja zaidi ya mara moja kati ya watu wawili waliokubaliana
kufanya hivyo.
Adhabu hiyo pia itatolewa kwa wale wanaopatikana
na hatia ya kuwahusisha watoto katika vitendo hivyo, walemavu au
kumuambikiza mtu virusi vya Ukimwi.
0 comments:
Post a Comment