Mkurugenzi
wa Kampuni ya Azimio, Mohamed Ikubal (mwenye kanzu) akitoa ufafanuzi
kwa wajumbe wa Bodi ya NSSF kwenye jengo la mauzo ya nyumba za mradi wa
Dege ECO Village, eneo hilo ndilo litakalokuwa likiendesha mauzo na
taratibu zote za mradi baada ya kukamilika.
Wajumbe
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)
jana wametembelea mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa unaojulikana kwa
jina la Dege ECO Village unaojengwa eneo la Kigamboni nje kidogo ya Jiji
la Dar es Salaam. Ujenzi huo wa mji wa kisasa ambao utakuwa na nyumba
za kuishi za kisasa za watu wa kipato cha kati unajumuisha ujenzi wa
nyumba zaidi ya 7,000 zikiwa na huduma zote za kujamii eneo moja.
Akizungumzia
mradi huo mkubwa unaotekelezwa kati ya NSSF kwa ushirikiano na kampuni
ya Azimio, Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi John Msemo aliwaeleza wajumbe
wa Bodi ya shirika hilo kuwa ujenzi wa makazi hayo ya kisasa kwa
wananchi wa kipato cha kati unaendelea vizuri.
Alisema
eneo hilo litakuwa na nyumba bora na za kisasa zikiwa na huduma zote za
msingi kwa jamii kama maduka, shule, hospitali, masoko, viwanja vya
michezi, kituo cha polisi, kituo cha zimamoto, eneo la ujenzi wa majengo
ya ibada, majengo ya burudani pamoja na miundombinu ya kisasa ya maji
safi na maji taka.
Alisema
ujenzi wa mradi huo wa kisasa utakapokamilika utakuwa na uwezo wa
kuchukua watu takribani elfu 30 ambao watapata makazi bora nay a kisasa
katika eneo hilo la Kigamboni.
Akifafanua
zaidi Mhandisi Msemo alisema ujenzi wa nyumba hizo utakuwa na awamu
tatu; ambapo awamu ya kwanza itakamilika mwaka 2016 ikiwa na nyumba
2,500, huku awamu ya pili ya ujenzi itakamilika 2017 ikiwa na nyumba
bora na za kisasa 2,500.
“…Awamu ya tatu tunatarajia ikamilike mwaka 2018 hii itakuwa na nyumba 2,460,” alisema Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi Msemo akifafanua zaidi kwa waandishi wa habari juu ya mradi huo.
Aidha
akijibu baadhi ya maswali ya wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa NSSF,
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dk. Ramadhan Dau alisema nyumba zote
zitakazojengwa katika mradi huo zitauzwa kwa watu wenye kipato cha kati
watakaohitaji. Alisema zipo zitakazouzwa kwa fedha taslimu na nyingine
kwa makubaliano ya mikopo kadri ya utaratibu utakavyotolewa na shirika
hilo pamoja na mwekezaji walieshirikiana naye kutekeleza mradi huo,
yaani kampuni ya Azimio.
Alisema
bei ya nyumba moja inakadiriwa kuuzwa kuanzia dola za Kimarekani elfu
80 hadi 130, na tayari wameanza kupokea fedha na maombi kwa
watakaohitaji au kulipa kidogo kidogo kwa utaratibu utakao kubalika.
Hata hivyo baadhi ya wajumbe wa bodi walipongeza juhudi za uongozi wa
NSSF kwa kubuni mradi huo wa kisasa ambao utawasaidia wengi na hivyo
kushauri kuna haja ya kutekelezwa na mikoa mingine.
0 comments:
Post a Comment