Katika siku
za karibuni, kumekuwepo na habari nyingi, baadhi zenye kuchanganya umma
na nyingine hata zikidai kuwa baadhi ya wafanyakazi nchini wanapanga
kuandamana endapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete atakubaliana na maombi ya nyongeza ya posho ya
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba .
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu (DPC), inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu habari hizo kama ifuatavyo:
(a) Kwamba
Mhe. Rais hajapata kupokea maombi yoyote kutoka kwa Uongozi wa Bunge ya
kumwomba aridhie kuongezwa kwa posho ya Wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba kutoka kiwango cha sasa cha sh. 300,000 (laki tatu)kwa siku hadi
kufikia sh. 500,000 (laki tano) ama sh. 700,000 (laki saba) kama ambavyo
imekuwa ikivumishwa katika baadhi ya vyombo vya habari.
(b) Na
kwamba kwa sababu Mhe. Rais hajapata kupokea maombi ya nyongeza ya
posho hiyo, hakuna ongezeko lolote la posho ambalo Mhe. Rais
ameliidhinisha.
(c) Kwamba
alichopokea Mhe. Rais ni maombi ya Uongozi wa Bunge wa kuomba Mhe. Rais
aridhie kufanyika marekebisho katika kiwango cha malipo ya siku kwa
Wajumbe hao cha sh. 300,000 (laki tatu) ili posho ya kikao iwe posho ya
kujikimu na posho ya kujikimu iwe ndio posho ya kikao.
(d) Kwamba
Mhe.Rais amelikubali ombi hilo la Uongozi wa Bunge la kufanyika kwa
marekebisho katika mpangilio huo wa posho lakini kiwango cha malipo ya
kila siku ya Wajumbe hao kibakie kile kile cha sh. 300,000 (laki tatu)
kwa siku.
(e) Kwamba
tayari Mhe. Rais amekwishaujulisha Uongozi wa Bunge kuhusu uamuzi wake
huo wa kukubali yafanyike marekebisho lakini kiwango kibakie kile kile
cha sh. 300,000 (laki tatu) kwa siku.
(f) Hivyo, Mhe. Rais hajaongeza kiwango cha malipo ya Wajumbe hao kwa sababu hakupata kuombwa wakati wowote kuongeza kiasi hicho.
Ni
matarajio ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, kuwa maelezo haya
ya ufafanuzi yatasaidia kufunga mjadala ambalo msingi wake kwa kweli
umekuwa haupo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
01 Machi, 2014
0 comments:
Post a Comment