Mabasi mengine 25 ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda),
yamekamatwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini na Baharini
(Sumatra), kutokana na kuendelea kukaidi amri ya kuwataka wafuate sheria
za usafirishaji wa abiria jijini.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa
Mfawidhi wa Sumatra, Conrad Shio alisema mpaka sasa wameshayakamata
mabasi 40, kati ya hayo, 15 yalikamatwa wiki iliyopita.
Madereva wa mabasi hayo wanadaiwa kufanya makosa
tofauti ikiwa ni pamoja na kutokuwa na leseni ya uchukuzi wa abiria
jijini Dar es Salaam, inayotolewa na mamlaka hiyo, stika na vibao vya
kuonyesha njia wanazokwenda.
Shio alisema walipoyakamata awali na kuyaachia,
uongozi uliahidi kutekeleza maagizo waliyopewa na Sumatra lakini
hawajayatekeleza mpaka sasa.
Alisema pia wamesitisha kwa muda kazi ya
kuyakamata na sasa wanaendelea na mazungumzo chini ya ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema baada ya mazungumzo hayo, atakuwa katika
nafasi nzuri ya kuweza kuzungumzia hatua zaidi ambazo watachukua au kile
ambacho watakuwa wameafikiana kwa vyombo vya habari.
“Tumeona tusitishe operesheni hii ya kuyakamata
mabasi haya ili kutoa nafasi ya mazungumzo chini ya ofisi ya Mkuu wa
Mkoa na iwapo mwafaka usipofikiwa tutajua cha kufanya” alisema Shio.
Kulingana na makosa ambayo yamekutwa katika mabasi
hayo, kila basi litalazimika kulipiwa Sh250,000 na kwa mabasi 40, Uda
watalazimika kulipia Sh10 milioni. Wiki iliyopita, Sumatra ilianzisha
operesheni ya kuyakamata mabasi ya Uda kutokana na malalamiko ya
wananchi kuwa yamekuwa yakivunja sheria na hayana stika wala vibao
vinavyoonyesha njia wanazopita.
0 comments:
Post a Comment